Na Theonestina Juma, Chato
CHAMA cha Ushirika wa Akiba na Mikopo Mshikamano (SACCOS) cha Wilaya ya Chato Mkoa wa Kagera kimetoa mkopo wa sh.bilioni 1.4 kwa wanachama wake kwa kipindi cha miaka minane iliopita.
Kwa mujibu Katibu wa Mshikamano Saccos, Bw. Charles Hussein mikopo hiyo ilitolewa kwa wanachama wapatao 506 na vikundi 16 tangu kuanzishwa kwake.
Bw. Hussein alisema sh. 1,004,161,050 zilitolewa kwa wanachama hao, ambapo tayari zimesharejeshwa sh. 705,688,775.
Alisema kati ya fedha hizo sh. milioni 298,471,375 bado ziko kwenye mzunguko wa miradi mbalimbali ya wanachama ambapo kiwango cha urejeshaji kinaridhisha.
Alisema mikopo wanayotoa inawekezwa katika sekta ya elimu, kilimo, biashara ndogo ndogo na uvuvi na kwamba kutokana na ziada inayotokana na shughuli ya ukopeshaji, Mshikamano Saccos inawalipia ada watoto watano wanaoishi katika mazingira magumu.
Bw. Hussein alisema Saccos hiyo ilioanzishwa mwaka 2003 na wanachama wake wamenunua hisa zenye thamani ya sh. 18,732,000 na wamejiwekea akiba ya sh. 227,367,815, inayoifanya iwe na mtaji sh. 246,990,415.
Alisema ili kuongeza huduma za kifedha karibu na jamii kwa lengo la kuwajengea tabia wananchi ya kujiwekea akiba, Saccos hiyo inaendesha akaunti ya amana, ambayo inatoa huduma kwa wanachama na wasio wanachama.
Alisema mbali na wanachama SACCOS hiyo ina jumla ya wateja 72 ambao hawana wanachama. Hadi Februari mwaka huu SACCOS hiyo imefikisha ya sh. 30,103,720.
Hata hivyo, Bw. Hussein alisema moja ya changamoto inayoikabili SACCOS yao ni pamoja na uhaba wa elimu ya ushirika kwa wanachama na jamii kwa ujumla.
Alisema kutokana na hali hiyo Saccos hiyo ina wadaiwa sugu 40. Kwa mujibu wa katibu huyo watu hao wanadaiwa jumla ya sh. 33,230,835 na kwamba baadhi yao wameshatakiwa mahakamani.
Mshikamano Saccos, inamilikiwa na kanisa la Kiinjili Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Magharibi.
No comments:
Post a Comment