Halmashauri ya Manispaa ina Kata 14, kati ya hizo Kata 6 ni za mjini kati ya hizo ni Bakoba, Hamugembe, Kashai, Bilele, Miembeni na Rwamishenye zenye mitaa 31 na Kata 8 ni za ukanda wa
kijani ambazo ni Kahororo, Buhembe, Nshambya, Nyanga, Kagondo, Kibeta, Kitendaguro na Ijuganyondo zenye Mitaa 35 na wakazi wengi wanaoishi kata za ukanda wa kijani ni wakulima na wafugaji, kaya zipatazo 7,346 zinajishughulisha na kilimo cha mazao mbalimbali, na kaya 1,992 ufugaji wa mifugo mbalimbali. Maeneo yote ya Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba yanapata mvua ya kutosha wastani wa 1200 mm kwa mwaka na kuruhusu uzalishaji wa mazao mbalimbali.
Hali ya kilimo
Mazao yanayolimwa ni migomba (Ndizi), viazi vitamu, muhogo na mahindi kwa mazao ya chakula, Kahawa, na Vanilla, kama mazao ya biashara. Eneo linalofaa kwa kilimo ni hekta 4,200 ambapo hekta 3,400 ndizo zinatumika kwa kilimo cha mazao ya bustani, chakula na biashara.
Malengo ya Kilimo msimu wa 2010/2011 kwa Manispaa
Idara ya kilimo ina lengo la kufikia ulimaji wa hekta 3,954 katika kata za ukanda wa Kijani na uzalishaji wa tani 14,171 za mazao ya chakula ambayo ni ndizi, mahindi, maharage, mihogo, viazi vitamu na mbogamboga pamoja na tani 514 za mazao ya biashara ikiwa ni vanilla na kahawa.
Mifugo:
Pamoja na kilimo cha mazao ya chakula na biashara, wananchi hujishughulisha na ufugaji wa mifugo aina mbalimbali. Mifugo inayofugwa ni pamoja na ng’ombe wa maziwa wapatao 2,580 , mbuzi wa maziwa 378 na asili 853, kondoo 74, Nguruwe 531, kuku wa kisasa 17,489, bata 654 pamoja na mifugo midogo kama Sungura na njiwa. Mazao yatokanayo na mifugo hii ni nyama, maziwa, mayai na ngozi.
Tatizo kubwa katika uzalishaji na mifugo ni magonjwa, katika kukabiliana na tatizo la magonjwa ya mifugo, wilaya imechukua hatua zifuatazo;-
Utoaji wa chanjo mbali mbali za mifugo unaendelea kutolewa, kutoa elimu kwa wafugaji juu ya kukabiliana na magonjwa kwa kutumia kanuni bora za ufugaji na kufanya tiba.
USHIRIKA
Wilaya ina chama Kikuu cha Ushirika KCU (1990) Ltd, katika Manispaa kinajihusisha na ununuzi wa Kahawa. Aidha, kuna benki ya wakulima ya Mkoa wa Kagera (KFCB LTD) inayotoa huduma ya mikopo kwa SACCOS na watu binafsi. SACCOS 34 zenye jumla ya wanachama 3,419 wakiwemo wanawake 2,006 na wanaume 1,413, SACCOS hizo zina Hisa zenye thamani ya Tshs. 73,246,071.00, pia zina akiba ya Tshs. 348,217,214.00, na Amana ya Tshs. 28,095,870.00.
Pamoja na hayo kipo chama cha ushirika cha ujenzi wa nyumba cha wanawake kilichoandikishwa kwa Na. KAR/674, kina jumla ya wanachama 176 na kina hisa zenya thamani ya Tshs. 10,420,000.00 na kina akiba ya Tshs. 8,372,000.00
Utekelezaji wa mpango wa kuendeleza sekta ya kilimo Wilayani (DADPs)
Halmashauri ya Manispaa inatekeleza miradi iliyo chini ya Mpango wa Maendeleo ya sekta ya Kilimo (Agricultural Sector Development Programme – ASDP) kupitia DADPs. Miradi ya kilimo inayotekelezwa na halmashauri ni pamoja na miradi ya uwekezaji katika kilimo, miradi ya kujenga uwezo na kuboresha huduma za ugani katika kilimo.
Kipaumbele kikiwa katika maeneo yafuatayo:
• Kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula kwa lengo la kuhakikisha usalama wa chakula kwa kaya
• Kuongeza kipato cha wakulima kwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya mbogamboga na matunda katika Kata za ukanda wa kijani
• Ujenzi wa masoko ili kurahisisha ukaribu wa masoko kwa wakulima
• Ujenzi wa miundombinu ya huduma za mifugo ili kuwa na mazao salama ya mifugo na ufuatiliaji na udhibiti wa magonjwa ya wanyama
• Kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa wataalam wa ugani ili kutoa huduma bora kwa wananchi.
• Kuongeza kipato cha wakulima kwa kuongeza ufugaji wa ng’ombe na mbuzi wa maziwa katika Kata za ukanda wa kijani
• Kuongeza kipato cha wakulima kwa kuhamasisha ufugaji wa kuku wa kisasa na uboreshaji kuku wa asili
• Kudhibiti magonjwa ya mifugo na kuongeza uzalishaji
• Kuwa na vyama vya ushirika vyenye kukidhi mahitaji ya kiuchumi na kijamii kwa wanachama.
• Kuanzisha vituo vya habari za kilimo ili kuongeza wigo wa habari na taarifa za kilimo kwa wakulima.
• Kuongeza thamani na kupunguza upotevu wa mazao kwa kuhimiza usindikaji wa mazao ya kilimo
Changamoto zinazoikabili sekta ya kilimo katika eneo letu ni pamoja na;
(a) Uharibifu wa mazao unaofanywa na wanyama waharibifu kama vile: - Ngedere na Panyabuku.
(b) Magugu sugu yenye mizizi mirefu (Rumbugu)
(c) Ukosefu wa eneo linalofaa kwa umwagiliaji.
(d) Upungufu wa rutuba ya udongo katika maeneo mengi ya Manispaa.
(e) Vijana kutopenda kujihusisha na shughuli za kilimo/Mifugo
(f) Maeneo ya kilimo kupungua kadri mji unavyopanuka.
(g) Magonjwa ya mazao na mifugo
(h) Kasi ndogo ya jamii kuchangia miradi yao ya maendeleo.
Katika kukabiliana na chngamoto /vikwazo wananchi wanaendelea kuelimishwa na kuhamasishwa juu ya kuchangia miradi yao ya maendeleo, elimu kwa wakulima na wafugaji inaendelea kutolewa juu ya kufuata kanuni bora za kilimo na ufugaji, hasa kwa kupitia vikundi vya wakulima vya Shamba Darasa, kusisitiza matumizui ya sheria ya nguvu kazi ( yaani kila mwenye uwezo wa kufanya kazi afanye kazi) na kuhamasisha uundaji wa vikundi vya udhibiti wa wanyama waharibibu kwa kila kata.
No comments:
Post a Comment