Askofu wa Dayosisi ya Karagwe Mh. Dr. Benson Bagonza akiwa na wageni walioitembelea dayosisi toka Sweden mapema mwaka 2011 (Picha na Mchg.Oscar Samwel).
Dayosisi ya Karagwe ni miongoni mwa dayosisi ishirini zinazounda Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania. Dayosisi ya Karagwe ilizinduliwa
rasmi tarehe 7/1/1979 pale Lukajange.Zifuatazo ni huduma za maendeleo ambazo hutolewa na Dayosisi ya Karagwe.
1. Huduma za Afya- Dayosisi ya Karagwe inamiliki Hospitali ya Nyakahanga ambayo ndiyo hospitali teule ya wilaya ya Karagwe.Hospitali hii ni mkombozi kwa jamii ya watu wa Karagwe na maeneo jirani kama wilaya mpya ya Misenye. Huduma za kinga na tiba hutolewa katika hospitali hii.Pia hutoa huduma nyingine kama huduma ya afya ya msingi, upimaji wa virusi vya Ukimwi kwa hiari (ANGAZA), kliniki kwa ajili ya akina mama waja wazito nk. Pia hospitali ya Nyakahanga inaendesha na kusimamia zahanati nyingine nne ambazo ni Nyakatera, Ibamba-Mabira, zahanati ya shule ya sekondari Karagwe na Katenga-Ngara.
2. Mradi wa kudhibiti Ukimwi- Kutokana na janga la ugonjwa wa Ukimwi unaowatesa watu wengi, dayosisi ya Karagwe iliamua kuanzisha mradi huu ili kuwasaidia watu katika jamii ya Karagwe kwa kuwapatia elimu juu Ukimwi, kusaidia yatima hasa kuwalipia karo na mahitaji mengine kwa kusaidiana na familia, kutoa chakula kwa wanaoishi na VVU pamoja na mambo ya haki na utetezi hasa kwa wajane ambao kwa njia moja au nyingine huwa katika hatari ya kukosa haki zao katika familia za waume zao.
Kilimo cha umwagiliaji Ihembe (Picha na Mchg.Oscar Samwel
3. Udiakonia na utetezi-Dayosisi ya Karagwe inawajibika katika kufanya shughuli za diakonia ikiwa ni kuwasaidia wasijiweza au watu ambao wanaishi katika mazingira hatarishi. Hapa makundi ya watu kama wazee, walemavu, wenye mtindio wa akili, nk husaidiwa katika kupatiwa mahitaji ya lazima ikiwemo chakula, mavazi, kuwajengea nyumba, kuwanunulia mashamba na kuwatetea wale walio katika hatari ya kukosa haki zao.Vilevile kitengo cha diakonia hutoa msaada wa mbuzi watano kwa kila familia iliyobainishwa kuwa maskini ili kwa njia hiyo mradi huo wa mbuzi uwasaidie kuongeza kipato cha familia ili waweze kujipatia mahitaji ya msingi pale nyumbani. Pia kitengo hiki cha diakonia hutoa elimu kwa jamii ili ione umuhimu na wajibu katika kuwasaidia wenye shida maana wanaishi nao katia jamii moja.
4. Elimu- Hii pia ni sehemu muhimu ya kazi ya dayosisi ya Karagwe. Mpaka sasa dayosisi ya Karagwe inamiliki shule mbili za Sekondari ambazo ni Shule ya Sekondari Karagwe (KARASECO) na Shule ya Sekondari ya wasichana Bweranyamge. Katika matokeo ya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2010 KARASECO imeshika nafasi ya pili (2) kimkoa kati ya shule 155 zenye idadi ya wanafunzi zaidi ya arobaini na ya 44 kitaifa kati ya shule 3196. Bweranyange imeshika nafasi 4 kimkoa kati ya shule 32 zenye wanafunzi chini ya 40 na ya 64 kitaifa kati ya shule 490. Pia dayosisi inamiliki shule mbili za kiingereza ambazo ni Tegemeo (English Medium) na Imani (English Medium). Vituo vingine vya elimu ni kama ifuatavyo: Chuo cha Biblia Nkwenda, Chuo cha ufundi na kilimo Nkwenda, Chuo cha ufundi staid kwa watoto yatima Lukajange, Chuo cha udiakonia na waalimu wa shule za awali Nkwenda. Pia katika upande wa elimu,dayosisi ya Karagwe inao mpango maalumu wa kuanzisha chuo kikuu hapa Karagwe na mipango inaendelea vizuri kwa matumaini kwamba chuo hiki kitaweza kuanza kupokea wanafunzi mwaka 2013 kama mipango yote itaenda kama ilivyopangwa.Ikumbukwe kwamba huduma zote za elimu hutolewa kwa watu wote bila kujali dini wala kabila.
5. Miradi ya Maendeleo: Dayosisi pia inasimamia miradi ya maendeleo kwa ajili ya jamii ya Karagwe na watu wengine wote kama ifuatavyo:Karagwe Hotel and guest house: Hiki ni kituo ambacho hutoa huduma za malazi chakula na ukumbi wa mikutano. Watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi hufurahia kutumia kituo hiki kwa sababu ya huduma zake bora, uaminifu wa wahudumu na utulivu uliop sehemu hiyo. Unafuu wa bei pia huwavutia watumiaji maana bei zetu zinalenga huduma zaidi kuliko biashara. Miradi mingine ni kama mashine za kusaga nafaka huko majimboni, miradi ya maji, upandaji miti, uwanja wa Ndege Ihanda, miradi ya wanawake ya kuinua kipato chao kama ufugaji wa kuku, ushonaji nk
6. Mradi wa utunzaji wa mazingira: Dayosisi ya Karagwe iko mstari wa mbele katika kutunza mazingira kwa kuamini kwamba mazingira ni uhai. Mradi huu unahusisha majimbo yote, sharika na mitaa ambapo inasisitizwa kwamba maeneo yote ya Kanisa yapandwe miti. Kwa mfano: Mwaka 2011 katika majimbo ya Mabira, Murongo, Bweranyange na Kyerwa jumla ya miti 500.000 ilipandwa chini ya mradi huu ambao uliazishwa mwaka 2004. Katika harakati hizi za utunzaji mazingira, dayosisi ya Karagwe kwa kushirikiana na Jimbo rafiki huko Ujerumani imeanzisha mradi wa mazingira uitwao KAKAUMAKI (Kampeni Kabambe ya Utunzaji mazingira Kituntu). Mradi huu unatekelezwa katika Jimbo la Kituntu na kwa mwaka jana jumla ya miti 17,500 ilipandwa. Pia dayosisi ya Karagwe inahimiza vituo vyake vyote ikiwemo mashule na vituo vingine kuhakikisha wanapanda miti kwa wingi ambayo mbali na kutunza mazingira lakini pia huko mbele ya safari itakuwa kitegauchumi pindi itakapovunwa.
7. Mradi wa Maisha mapya (New life in Karagwe) Huu ni mradi ambao ulianzishwa mwaka 2006 na unalenga kuwawezesha wanajamii kubadili maisha yao toka hali duni ya kipato hadi kupata hali nzuri na kumudu kutunza familia zao. Mradi huu unahusika na kuwasaidia wakulima waweze kulima kwa kutumia mbinu za kisasa ambapo mkulima hupewa Ng’ombe mmoja jike ili pamoja na kupata maziwa lakini pia mkulima hupata mbolea kwa ajili ya shamba lake na hivyo kipato cha familia kuongezeka. Upande wa wanawake wajane wao hupewa mbuzi wa maziwa. Mpaka sasa jumla ya Ng’ombe 300 na mbuzi 100 tayari wamegawiwa kwa walengwa. Pia semina hutolewa kwa wakulima jinsi ya kulima kwa tija na kutunza mazingira. Wakulima hupata nafasi ya kutembelea maeneo ya kilimo ili kujifunza kwa vitendo.Mfano mwaka 2010 wakulima walitembelea Maruku Bukoba na Igabiro ambapo walipata nafasi ya kujifunza kwa vitendo. Kadhalika mradi huu unawaelimisha watu juu ya utunzaji mazingira
9. SACCOS: Huu ni mpango wa kuwasaidia wananchi ili waweze kuweka na kukopa kupitia vikundi vyao vya SACCOS ambao ulianza rasmi mwaka 2009. Mpaka sasa jumla ya Saccos 8 tayari zimesajiliwa katika majimbo ya Ihembe na Bweranyange. Kitengo cha Saccos ambaocho kiko makao makuu ya dayosisi Lukajange huwasaidia wanachama kuwapatia elimu kwa njia ya semina, kuwapa vitendea kazi hasa wakati wa kuanza kama vitabu, kasiki, nk. Pia kwa sasa wako katika kuziwezesha Saccos hizo kujenga ofisi za kuduma ambapo kikundi husaidiwa kupewa mabati, sementi, milango na madirisha ya chuma,vifaa vingine ni mchango wa wanachama.
No comments:
Post a Comment